Website counter

Home Picha Habari Siasa Michezo na Burdani Niandike Email: sugumalaria@gmail.com  

AMANI NA UTULIVU NDIO MSINGI WA MAENDELEO

 

 

 

 

 

 

 

TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA
Magazeti Yetu
Kutoka Mitandao Mengine
Vyuo Vikuu
 
 
 
 
 
 

 

 

 

 

 

Zitto adaiwa kuhongwa kuitetea CHC

 

 

WAZIRI kivuli wa Wizara ya Fedha, Zitto Kabwe na wajumbe wa Kamati ya Mashirika ya Umma wamedaiwa kuhongwa sh milioni 60 ili walitetee shirika hodhi la mali za umma (CHC).

Tuhuma hizo zilitolewa jana na mbunge wa viti Maalum, Anastazia Wambura, ambaye alisema kuna baadhi ya wabunge ambao wanaitetea CHC ili lipewe muda zaidi.

Wambura alitaka serikali itoe kauli juu ya jambo hilo kwani linadhalilisha Bunge na serikali.

Katika majibu yake Mkulo alikiri kupokea tuhuma hizo na wamewaomba Mdhibiti na Makaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali CAG azifanyie kazi.

“Nimesikia rushwa waliyopewa ni sh milioni 60, hili la rushwa lilitajwa hapa bungeni, tumemuomba CAG achunguze madai kuwa kuna rushwa ilitembea kushawishi CHC lipewe muda wa kudumu badala ya muda uliopendekezwa na serikali.

Awali Zitto, alisema yuko tayari kujiuzulu uenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu ya Mashirika ya Umma (POAC) na ubunge iwapo itathibitika kuwa yeye au mjumbe wa kamati yake amehongwa.

“Naomba uchunguzi wa tuhuma hizo ufanywe kwa uwazi na endapo zitathibitika kuwa na ukweli mimi niko tayari kujiuzulu ubunge na uenyekiti wa kamati,” alisema.

Zitto alisema anazo hadidu za rejea kutoka bodi ya CHC kwenda kwa CHC na amemuomba Mkulo na Waziri wa Utawala Bora aiagize Takukuru ifanye uchunguzi.

“Uchunguzi huu utangazwe na uwekwe wazi, Waziri Mkulo aahidi kuwa ikigundulika amesema uzushi na uongo mara moja ajiuzulu,” alisema Zitto.

Zitto pia alimtaka Mkulo kuhakikisha kuwa hadidu za rejea zinazopelekwa kwa CAG zinafanyiwa marekebisho ili aweze kuzichunguza  na kuweka wazi matokeo ya uchunguzi huo.

“Namuomba Waziri Mkulo aweke ahadi mbele ya Bunge kuwa atajiuzulu kama nitakavyofanya mimi endapo matokeo ya uchunguzi huo yatagusa pande zetu kulingana na tuhuma zilivyotolewa,” alisema.

Waziri wa Fedha Mustafa Mkulo, alikana kuziona hadidu za rejea zilizoandikwa na bodi ya CHC kwenda kwa CAG.

“Mheshimiwa Zitto tuhuma hizi ni nzito ndiyo maana nikasema zitafanyiwa kazi kwani serikalini tuna utaratibu wa kuviagiza vyombo vya serikali kufanyia kazi mambo mazito,” alisema.

“Utaratibu wa kujiuzulu unatokea kwa namna mbili kwanza tungesubiri uchunguzi ufanyike, taarifa ipatikane halafu lije suala la mtu kujiuzulu ama kutojiuzulu,” alisema.

Mkulo alisema baada ya uchunguzi huo wa CAG taarifa itapelekwa bungeni mara moja.

Juni 23 wakati Bunge lilipokuwa likijadili Muswada wa Mabadiliko ya Sheria ya mwaka 2011, Zitto alipinga kauli ya serikali iliyowasilishwa na Mkulo na kudai Baraza la Mawaziri limerubuniwa ili kuliua CHC.

Katika maelezo yake, Zitto alisema kipengele cha kuhamisha kazi za CHC kilikataliwa na Kamati ya Fedha na Uchumi kwa kuwa kuhamishia kazi za CHC katika Ofisi ya Msajili wa Hazina kulilenga kuyaua mashirika ya umma nchini.

 

 

 

Zitto na Demokrasia

KUONDOA MGAWO WA UMEME TANZANIA

Mpango mzuri, Fikra pungufu kidogo

Zitto Kabwe

Taifa zima lilikuwa linasubiri siku ya tarehe 13 Agosti 2011 ili kufahamu ni jambo lipi jipya Waziri wa Nishati na Madini atakuja nalo kuhusu kumaliza tatizo la mgawo wa Umeme nchini. Tangu mwaka 2006, Tanzania imekuwa ikipata tatizo hili kwa wastani wa kila mwaka isipokuwa mwaka 2007 na 2008 kipindi ambacho Shirika la Umeme nchini TANESCO lilikuwa linanunua umeme kutoka mitambo ya Kampuni za Aggreko na Dowans. Mwaka 2009 adha ya mgawo ilikuwa kubwa sana, ikaendelea mwaka 2010 na baadaye mwaka 2011. Mamlaka ya Mapato nchini walikadiria kupoteza zaidi ya shilingi 840 bilioni kama kodi kutokana na mgawo wa mwaka 2011 peke yake. Hakuna hesabu zilizowekwa wazi kuhusu mgawo wa mwaka 2009 na ule wa mwaka 2010. Pia wachumi wa Tanzania hawajaweza kutueleza katika kila mgawo unaotokea nchini ni kwa kiwango gani ukuaji wa Pato la Taifa unaathirika. Kwa mfano, ukuaji wa sekta ndogo ya Umeme ukiporomoka kwa nukta moja, ukuaji wa uchumi unaathirika kwa kiwango gani. Taarifa kama hizi zinaweza kusaidia sana watunga sera kuweza kujua umuhimu wa sekta ndogo ya Umeme katika juhudi za kukuza uchumi na kuondoa umasikini nchini.

Mwaka 2011 ulianza kwa Kamati za Bunge za Nishati na Madini na ile ya Mashirika ya Umma kuweka kipaumbele katika uzalishaji wa Nishati ya Umeme. Kamati ya Mashirika ya Umma ilijikita katika kuhakikisha Uzalishaji wa Umeme wa uhakika kutoka katika vyanzo vya Makaa ya Mawe (Mchuchuma, Ngaka na Kiwira).

Kamati ya Nishati na Madini Ilijikita katika kuhakikisha Wizara inasimamia vya kutosha sekta ndogo ya Umeme na kumaliza kabisa tatizo la Mgawo wa Umeme katika muda wa mfupi, wa kati na mrefu. Kutofanikiwa kwa juhudi hizi na hasa kutoonekana kwa Bajeti ya kutosha ya Sekta hii kulifanya Bunge likatae kupitisha Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini.

Hatimaye Serikali ilileta Mpango wa Dharura ulioitwa Mkakati wa kuondoa Mgawo wa Umeme na kuimarisha Sekta ndogo ya Umeme. Mkakati huu ni wa miezi 16, kuanzia Agosti 2011 mpaka Disemba 2012. Mkakati huu utakagharimu jumla ya Shilingi 1.2trilioni. Fedha nyingi sana lakini kwa matumizi muhimu sana ya kulihami Taifa. Kimsingi hii ni ‘stimulus package’ kwa Sekta ya Umeme!

Mkakati huu utaingiza jumla ya 882MW za Umeme katika gridi ya Taifa ifikapo mwezi Disemba mwaka 2012. Katika hizi 572MW zitaingia katika Gridi mwezi Disemba 2011. Jumla ya 422MW zitatokana na Mashine za kuzalisha Umeme za kukodisha kutoka Kampuni mbalimbali binafsi (37MW Symbion, 80MW IPTL, 100MW Aggreco, 205MW Symbion II ). Mradi pekee ambao tunaweza kusema ni wa ndani ni ule wa 150MW ambao utamilikiwa na Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF).

Shirika la NSSF liliomba Serikalini kuingia katika uzalishaji wa Umeme toka mwaka 2010 kufuatia maelekezo ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma. Juhudi zake zilikuwa zinagonga mwamba kutoka kwa watendaji wa Wizara ya Nishati na Madini kwa sababu ambazo hazijaelezwa waziwazi. Kwa hatua ya sasa iliyo kwenye Mkakati, Tanzania italipa Kampuni binafsi za nje zaidi ya Shilingi 523 Bilioni kutokana na kununua Umeme kutoka katika mitambo yao. Ingewezekana kabisa NSSF wangeombwa kuwekeza zaidi na hata kuwaomba Mashirika mengine kama PSPF kuwekeza na kupunguza kulipa fedha za kigeni kwa kampuni za nje.

Serikali itatoa dhamana (guarantee) kuiwezesha TANESCO kuchukua mkopo wa 408 bilioni tshs kutoka katika Mabenki ya ndani. Sekta Fedha nchini itabidi iandae ‘syndicated’ mkopo mwingine kwa TANESCO zaidi ya ule wa mwanzo wa mwaka 2007 wa tshs 300 bilioni ambazo ninaamini unalipwa bila ya mashaka. Hivi Serikali isingeweza kuuza Bond ya thamani hiyo? Wataalamu wa fedha wataweza kulijuza Taifa njia bora zaidi ya kupata fedha hizi. Hata hivyo Sekta ya Fedha ni moja ya sekta zitakazo faidi Mkakati huu, ikiwemo Sekta ndogo ya Mafuta (kwa kuuza mafuta ya kuendesha mitambo). Sekta ndogo ya Usafiri pia nayo itafaidika kwa kusafirisha mafuta kutoka Bandari ya Dar es Salaam kwenda kwenye mikoa ambayo Mitambo ya kuzalisha umeme itawekwa kama Tanga, Dodoma, Mwanza na Arusha.

Ifikapo Mwezi Disemba 2012 Tanzania itakuwa imeongeza 310MW za Umeme ambazo zote zitakuwa zinamilikiwa na Shirika la Umeme au 150MW kati ya hizo Shirika la NSSF. Kwa maana hii ni kwamba katika jumla ya Uzalishaji wa Umeme wa 882MW  tunaotarajia kuongeza katika Gridi ya Taifa, utakaobakia nchini baada ya Mashine za kukodi kuondoka ni 460MW peke yake. Tutatumia  tshs 1.2tr kuingiza katika Gridi wa umeme wa kudumu wa 460MW tu. Hii inatokana na ukweli kwamba baada ya Disemba 2012 jumla ya 422MW zitakuwa zimeondoka kwenye Gridi baada ya mikataba ya kukodisha kumalizika.

Jambo moja zuri  ni kwamba Serikali imefikiri kimkakati kwamba tuwe hatuna mitambo ya kukodi ifikapo Disemba 2012 (kwa maana ya symbion na Aggreco). Huku ni kufikiri vizuri, kwamba Serikali itakuwa  imejenga uwezo wa Taifa kupitia TANESCO na NSSF kuwa na uwezo wa kuzalisha umeme wake. Imefanya ‘sequencing’ kwamba itatumia umeme wa kukodi wakati inajenga uwezo wa kununua mitambo yake yenyewe. Wakati Mikataba ya kukodi inakwisha, ndani ya miezi 16 Serikali kupitia TANESCO na NSSF itakuwa inazalisha 460MW. Hatua ya kupongeza.

Hata hivyo, Serikali na wananchi wanapaswa kujiuliza katika hiki kipindi cha mpito jambo gani litakuwa linafanyika? Ifikapo Disemba mwaka 2012 kutakuwa na mahitaji zaidi ya Umeme kwa ziada ya 200MW au zaidi. Hii inatokana na ukweli kwamba mahitaji ya umeme yaliyopo hivi sasa ni ‘suppressed’ licha ya ukuaji wa asilimia 15 kila mwaka. Vile vile inatarajiwa  kuwa kuwepo kwa umeme kutaongeza uzalishaji ambao utaongeza mahitaji zaidi. Hapa Serikali ilifikia ukomo wa kufikiri (ilichoka). Kunapaswa kuwa na kazi inayofanyika ambayo inafikiri zaidi ya 2012 (Thinking Beyond Dec 2012). Kunahitajika mradi wa angalau 200MW kuanza kutekelezwa kati ya sasa na Disemba 2012 ili mitambo ya kukodisha ikiondoka kuwepo na uwezo wa angalau 600MW. Hapa ndipo Mradi wa Kiwira I unaingia.

Mkakati wa Serikali kwa KIWIRA una makosa ya kifikra. Serikali inataka kukopa Uchina ili kujenga Kiwira. Mchakato wa mkopo utachukua zaidi ya miaka 2. Taifa haliwezi kusubiri. Serikali iharakishe utwaaji wa Hisa za Kampuni ya TanPower Resources na kukabidhi hisa hizo kwa Shirika la Umma. Shirika litangaze Zabuni kupata ‘strategic investor’ kwa utaratibu wa PPP ambao utazingatia kwamba mara baada ya Mwekezaji kujilipa gharama zake na faida kidogo umiliki uwe sawa kwa sawa (50/50).

Licha ya Mkakati kuendeshwa na zaidi na fedha za mikopo kutoka katika Mabenki, bado umepangwa vizuri mpaka 2012. Hata hivyo, Mkakati wa kuondoa mgawo wa Umeme na kuimarisha sekta ndogo ya Umeme nchini haukufikiriwa vya kutosha (inadequate thinking) na hasa kwa mbele ya 2012. Bado kuna fursa ya kuboresha. Kamati za Bunge za Nishati na Madini na Mashirika ya Umma zinapaswa kufuatilia kwa karibu sana utekelezaji wa Mkakati huu.

Mbio za ubunge Igunga Dkt. Slaa, Zitto kuzindua kampeni

*CHADEMA kutumia helikopta Igunga
*Yaanika mikakati ya kushinda jimbo
*CCM yavuta pumzi, yasubiri CC


Na Benjamin Masese

VUGUVUGU la uchaguzi mdogo wa Jimbo la Igunga, mkoani Tabora linazidi kupanda
huku Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kikitangaza safu ya viongozi wa kitaifa watakaozindua kampeni za chama hicho Septemba 9, mwaka huu.

Mbali na kuanika majina ya viongozi wake watakaozindua kampeni, chama hicho kina mkakati wa kutumia helikopta ili kufikia maeneo yote ya Jimbo la Igunga.

"Kama kawaida yetu tayari  helikopta imeandaliwa kwa mashambulizi ya kampeni jimbo la Igunga, lakini hatutaanza nayo, tutaanza na vyombo vya ardhini kwanza tukiona kuna ulazima, ndipo tutakaponyanyuka juu kwa juu na kumwaga sumu 'chini'."

Hayo yalisemwa na Mkurugenzi wa Habari Mawasiliano na Uenezi wa CHADEMA, Bw. Erasto Tumbo, wakati akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu akiwa Igunga. Alisema viongozi wa kitaifa watakaohudhuria uzinduzi wa kampeni za chama hicho ni Katibu Mkuu, Dkt. Willbroad Slaa na Naibu Katibu Mkuu Bw.Zitto Kabwe.

Bw. Tumbo alisema kuwa tayari Kamati Kuu ya CHADEMA ilikutana juzi na kupitia majina ya wagombea 16 waliochukua fomu, ambapo kwa kuzingatia sifa na mtu mwenyewe anavyokubalika kwa wananchi wa Igunga, ilimpitisha Bw.Joseph Kashindye, kuwania kiti hicho.

"Hapa tulipo hatujaanza kampeni, lakini wananchi wameonesha shauku kubwa ya kukiunga mkono chama chetu ili kuwaongoza, kwani wamedai kwamba kwa miaka mingi walikuwa hawajapata kiongozi wa kukaa nao na kujadiliana wanachohitaji," alisema Bw. Tumbo.

Alisema baada ya uzinduzi huo viongozi wa kitaifa watasambaa maeneo yote ya jimbo hilo kumnadi mgombea Bw. Kashindye, ili kuhakikisha jimbo hilo linaondoke mikononi wa CCM).

Alisema utafiti wa awali umeonesha kuwa  CHADEMA itaibuka na  ushindi kwa zaidi ya asilimia 80, huku vyama vingine vikigawana asilimia zilizobaki.

Alisema CCM ina hali mbaya kuliko vyama vingine vinavyoshiriki uchaguzi huo. Alisema dalili zinaonesha kuwa wananchi wamechoka na sera za chama hicho.

"Hadi sasa tunajua tunashinda na harakati za kumwaandaa mgombea wetu kwenda bungeni zimeanza na tutampeleka kwa maandamano hadi Dodoma na kufanya hafla fupi ya kumkaribisha,"alisema.

Naye Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa Itikadi na Uenezi, CCM Bw. Nape Nnauye, alisema muda wowote kuanzia sasa Kamati Kuu itakutana kumteua mgombea wa chama hicho na kutangaza siku ya kuanza kampeni.

Akizungumza na gazeti hili jana,Bw. Nnauye alisema kauli za CHADEMA kujihakikishia ushindi ni mbinu za kuwatisha watu na wagombea wengine, lakini CCM inazichukulia kama kelele ambazo zimezoeleka kwao.

"Hakuna chama ambacho kinatangaza mikakati yake  barabarani,tunatarajia Kamati Kuu itakaa muda wowote kumpitisha mgombea mmoja na kutangaza siku rasmi ya uzinduzi wa kampeni, wao ndio wanasuasua sisi tuko imara na ushindi ni wetu kama kawaida,"alisema.

Awali alisema CCM ina asilimia 90 za ushindi katika jimbo hilo na kuongeza kwamba  kampeni za chini chini za baadhi ya vyama vya siasa zilizoanza Igunga ni mchezo wa watoto wadogo.

"Pale Igunga, CHADEMA haina kitu hata kama wameanza kampeni za chini chini...ule ni mchezo wa watoto na kawaida ikifika saa sita usiku lazima watoto walale na ndipo tutakaposhinda. Pia tathmini tulishafanya na tumebaini zaidi ya asilimia 90 tunashinda ndio maana hatuna wasiwasi,"alisema.

Naye Rachel Balama anaripoti kuwa  Chama cha Wananchi (CUF) kinatarajia kutangaza ratiba na mikakati mingine leo.

Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu akiwa Igunga, Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Bara), Bw. Julius Mtatiro, alisema;

"Nipo Igunga kwa ajili ya maandalizi ya uchaguzi, lakini kesho nitatoa taarifa zote kuhusu kampeni za CUF."

Naye Mwenyekiti wa Chama cha National Reconstruction Alliance(NRA) Bw. Rashid Mtuta, alisema kuwa chama chake kina nia ya kusimamisha mgombea na kinasubiri timu iliyotumwa Igunga kuangalia mazingira ya kukubalika kwake jimboni humo.

Alisema tayari timu hiyo ya watu watano ipo kwa wiki moja sasa na inatarajia kurudi wakati wowote kuanzia leo.

"Tunapozungumza tayari timu ya watu watano ipo Igunga kuangalia mazingira na tutatoa tamko," alisema Bw. Mtuta.

Alisema kuwa timu hiyo inaonngozwa na Kaimu Katibu Mkuu Taifa Bw.

 

 

 

 

Copyright © 2011 Malaria Sugu. All rights reserved.  

 

 

 

 

Free Web Hosting